UPO NDANI YA MOYO HUU MTAKATIFU WA YESU?


Na Josephat Leander Kabutta, S.J.

UTANGULIZI:
Neno ‘Moyo’ katika maisha yetu lina matumizi mengi. Mara nyingi tumesikia watu wakisema:
· “Yule dada ana Moyo mwema”.
· “Ana Moyo wa huruma”.
· “Maneno yake nimeyatunza Moyoni”
· “Mzee yule ana Moyo baridi sana!”
· “Nakupenda kwa Moyo wangu wote”.
· “Alitupa Moyo, tukaendelea na kazi”.
· “Madharau yake yametuvunja Moyo”.

Watu hutumia neno Moyo wakiwa na maana ya nia, Makusudio, Upendo mkubwa na zaidi “kile kinachowasukuma kutenda jambo. Basi si vibaya nikisema:
· “Moyo mwema humsukuma mtu kutenda mema”.
· “Moyo wa mapenzi humsukuma mtu kupenda”.
· “Moyo mbaya humsukuma mtu kutenda mabaya”.
· “Moyo wa kazi humsukuma mtu kufanya kazi bora bila kukatishwa tamaa kirahisi”.
· “Moyo uliovunjika huleta huzuni na masikitiko”.

Labda tufikiri:
· “Ni nini kilichomsukuma Kristu kuja duniani na kuchukua mwili wa kibinadamu?”
(Yoh. 1:14)”
· “Ni nini kilichomsukuma Yesu kuihubiri Injili? (Mat. 4: 17).
· “Ni nini kilichomsukuma Yesu kuwafukuza wafanyabiashara Hekaluni?” (Mat. 21: 12-13; Mar. 11: 15-17; Luk. 19: 45-46; Yoh. 2: 13-17).
· “Ni nini kilichomsukuma Yesu kuponya wagonjwa na kusamehe dhambi?” (Mat. 12: 9 - 13).
· “Ni nini kilichomsukuma Yesu kuwaonea watu huruma, kuwafundisha na kuwalisha?”(Soma: Marko 6: 33-44).
· “Ni nini kilichomsukuma Yesu kusalitiwa, kuteshwa na kuuawa kikatili Msalabani?” (Marko 14: 32 - 15: 1 - 40).

Hakika jibu ni moja tu: ni moyo wake au twaweza kusema ni upendo wa moyo wake. Upendo huu umejionyesha katika Agano la Kale, Injili, Matendo ya Mitume, Mafundisho ya Mitume na Kanisa lake. Ni Moyo uliotupenda sana:
“Maana Mungu aliupenda Ulimwengu hivi hata akamtoa mwanae wa pekee ili kila anayemwamini asipotee, bali awe na uzima wa milele,” (Yoh, 3:16).

Hivyo ni Moyo wa Yesu (Mtakatifu) ndio uliomsukuma kuja duniani katika hali duni, kutuponya magonjwa, kutuletea msamaha wa dhambi na kufa kwa ajili yetu - Kufa ili sisi tupate uzima.

Moyo wake kwa asili ni Moyo wa Upendo na matunda ya upendo wa moyo wake ni huruma, unyenyekevu, upole, msamaha wa dhambi, na kikubwa zaidi ni Wokovu.
MOYO WA YESU:
Yesu alisema haya kuhusu Moyo wake:
· “Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na kulemewa na mizingo, nami nitawapumzisha.
· Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu.
· Maana, nira yangu niwapayo ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”. (Mat. 11: 28-30).
Yesu anatuita sote katika Moyo wake tupate tulizo. Tukijitoa kwake, yeye ataondoa mabaya (mizigo) katika mioyo yetu na kutuwekea wepesi. Maisha yetu yatajaa furaha, upendo na matumaini. Tuujie Moyo wake mpole na mnyenyekevu na kutoka katika hazina ya moyo wake tutapata mema yote pasipo kipimo. Yesu alisema:
“Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa mabaya katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake....” (Luka 6: 45).

Je! Kuna aliye mwema kuliko Yesu? Hakuna. Ndiye aliyetupenda sana hata kutoa uhai kwa aibu kwa ajili yetu. Ndiye aliyetufundisha upendo kwa hali ya juu kwa mafundisho na maisha yake. Alituasa tuwapende hata adui zetu.

“Lakini nawaambieni ninyi mnaonisikiliza, wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang’anya koti lako mwachie pia shati lako”. (Luka 6: 27-30).

Kweli ni upendo wa ajabu aliotufundisha Yesu. Je! unawezekana katika maisha? Ndiyo unawezekana - “hakuna lisilowezekana kwa Mungu”. Kumbuka alivyosema kuhusu kulinganisha uwezo wa Mungu na Mwanadamu: Kwa mwanadamu haiwezekani kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano, lakini kwa Mungu, yote yawezekana (Soma Luka 18:25-27) Labda kwa binadamu ni shida kwa kuwa:
“Mawazo ya Moyo wa Mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake...” (Mwanzo 8: 21)

Lakini Yesu aliweza kuuishi upendo huu, japokuwa alikuwa na ubinadamu kama wako na wangu; kumbuka pale Msalabani aliwaombea wale waliomsulibisha:
“Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui wanalofanya” (Luka 23: 34).

Ili basi tuuishi Moyo huu, hatuhitaji moyo wa binadamu, moyo uliojaa makusudio mabaya, bali tunahitaji Moyo wa
Mungu - ndio Moyo wa Yesu. Sharti tumpe mioyo yetu ataiondoa na kutupa moyo wake yeye aliahidi:

· “Nami nitawapa Moyo, wanijue ya kuwa mimi ni Bwana; nao watakuwa - watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; kwa maana watanirudia kwa Moyo wao wote.” (Yeremia 24: 7).

· “Nami nitawapa Moyo mmoja, nami nitatia roho mpya ndani yao; nami nitauondoa moyo wa jiwe katika miili yao, nami nitawapa moyo wa nyama; ili waende katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyatenda; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao.

Kumbe ili kuuishi upendo huu wa Kristu twauhitaji moyo wake! Kwa moyo wetu wa kibinadamu - mgumu na baridi kama jiwe hatuwezi. Basi hapa waweza kujifunza faida za kujiweka katika moyo wake:
· Tutamjua na kumkiri kweli kuwa yeye ni Bwana nasi tu watu wake aliowaumba, akawakomboa, na anawapenda upeo.
· Tutakuwa wamoja katika roho na upendo wake. Yaani tutakuwa viungo vya mwili wake - Kanisa lake.
· Tutazishika vema amri za Mungu - wala hatutaona mzigo kuzishika bali baraka na fahari yetu.
· Tutaishi kweli kama watoto wa Mungu, tukiwa na matumaini ya kuwa naye milele.
· Hakuna chochote kile kitakachoweza kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kuuawa?” (Rom. 8: 35).

Tutawezaji basi kuingia katika Moyo wa Yesu, na hivyo kustahili hazina za Moyo wake? Yeye asema “Njooni kwangu ....”, twende vipi? Njia iko wapi?

Twaweza kuuendea Moyo wa Yesu: Kwanza kwa kutambua kuwa sisi tu wadhambi, kuona uchungu kwa dhambi zetu ... yaani kutambua kuwa mioyo yetu haifai. Tunaambiwa:
“Lakini hata sasa nirudieni kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza; rarueni mioyo yenu na si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma, naye hughairi mabaya. (Yoeli 2: 12- 13).

Naam, sisi tu wachafu na mioyo yetu imejaa uchafu. Tusikate tamaa tukazani hatusafishiki wala mizigo yetu haichukuliki. Yeye anasema, “Njoni ninyi wote msumbukao na kulemewa ... nitawapumzisha”. Tena asema:
“Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana.
Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu”. (Isaya 1:18).
Yeye Yesu amekwishachukua mizigo yetu yote na kubeba dhambi zetu pale Msalabani. Nabii Isaya alitabiri, na ikiwa kweli kuwa:
“Hakika ameyachukua masikitiko yetu,
amejitwika huzuni zetu:
Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa.
Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu,
Alichubuliwa kwa maovu yetu;
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na
kwa kupigwa kwake sisi tumepona. (Isaya 53: 4-5).

Kisha, baada ya kutubu na kupokea utakaso - yaani moyo wa jiwe kuondolewa ndani mwetu, sasa tumwache atupe moyo wake, ndio moyo wa upendo. Upendo uwe kanuni ya maisha yetu, mwongozo wetu, sheria yetu, sababu ya uhai wetu na tulenge kupenda zaidi na zaidi (Soma kitabu cha Kumfuasa Yesu Kristu - mada za upendo). Tumpende nani? Vipi?
“Mpende Bwana Mungu wako kwa Moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe”. (Luka 10: 27).

Lakini jirani yako ni nani? (Soma Luka 10: 29 - 37).

Mafundisho mengine kuhusu upendo waweza kuyapata:
Mathayo 5: 43 - 46/6: 24/19: 19/22: 37 - 39.
Marko 12: 30 - 33.
Luka 16: 13.
Yohana 3: 16 - 19/3: 35 - 36/15: 5 - 17.

Tena tutampendaje Yesu? Tutampenda kwa kufanya anavyotaka - kuishi Kikristu kama alivyotuamuru.Yesu alisema:
“Mkinipenda mtazishika amri zangu”. (Yoh. 14:15).
Nazo/nayo amri yake ndiyo hii:
“Pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi. Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu (Yoh. 13: 34- 35).

Kumbe basi kuuingia moyo wa Yesu ni Kumpenda Mungu na jirani, na kumpenda Mungu ni kushika amri zake, na amri yake ni kupendana kama alivyotupenda yeye! Yote yanazunguka katika upendo na Upendo ni yeye mwenyewe! “Mungu ni upendo, tupendane”.

Baada ya kumpenda Mungu, tudumu katika upendo huo. Tukiacha kupenda tunajitoa katika Moyo wake Mtakatifu, na ole wetu akitukuta tukiwa nje.

Tujifunze kupenda kikweli, upendo wa kweli:
· hauhesabu mabaya,
· haujivuni
· haukati tamaa
· haushindwi na shetani
· hausitisiti
· hauna mwisho wala kikomo
· hauangalii rangi
· hauangalii kabila wala lugha
· haubanwi na sheria
· haulali wala kusinzia
· hauuziki wala hauna bei - hutolewa bure
· hauna hasira
· hauna woga
· haukasiriki wala kukunja uso
· upo wakati wote, popote, vyovyote na kwa wote.

Somo kuhusu kupenda na kudumu katika pendo:

“Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu. Mtu asiye na upendo, hamjui Mungu, maana Mungu ni Upendo. Na Mungu alionyesha upendo wake kwetu kwa kumtuma mwanaye wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uzima kwa njia yake. Hivi ndivyo upendo ulivyo: Si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma mwanae awe sadaka ya kuondolewa dhambi zetu”.

Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana. Hakuna mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana, Mungu anaishi katika Muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu.

“Mungu ni Upendo, na kila aishiye katika upendo, anaishi katika Muungano na Mungu na Mungu anaishi katika Muungano naye. Upendo umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri siku ili ya hukumu, kwani maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristu. Palipo na upendo hapana uoga; naam, upendo kamili hufukuza uoga wote. Basi mtu mwenye uoga hajakamilika katika upendo, kwani uoga huhusikana na adhabu.

“Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza. Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia ndugu yake, huyo ni mwongo. Maana mtu asipompenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hamwoni. Basi hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda Ndugu yake”. (1 Yoh. 4: 7 - 21).

Basi ni katika kupenda ndiyo tunakuwa ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, na Moyo Mtakatifu wa Yesu, unakuwa ndani yetu, nao unatuwezesha kupenda kikweli na kudumu katika kupenda.

KUWEMO KATIKA MOYO MTAKATIFU WA YESU
Moyo Mtakatifu wa Yesu ulitobolewa pale Msalabani kwa mkuki. Vyote vilivyokuwa ndani vikamwagwa kwetu nje ... navyo ni maji kututakasa na damu kutuokoa. (Yoh. 19: 34, Efes. 1: 7).

Moyo wake umeachwa wazi, na yeyote ana ruhusa ya kuingia, tena aliyeingia ana ruhusa ya kutoka!
Uwapo ndani ya Moyo wake, bado ukazidi kuzivunja amri za Mungu, unamuumiza zaidi kuliko ukiwa nje. Hebu jiulize ikiwa mdhambi anauumiza Moyo Mtakatifu wa Yesu akiwa nje, akiwa ndani Je?

Basi tufanye haya tukishaingia ndani ya Moyo mtakatifu wa Yesu.
· Tuwache dhambi na tutende mema kwa wenzetu, hata maadui zetu; Tena tuwaeleze wenzetu kuhusu upendo huu wa Mungu: Soma Waef. 5: 1- 14.
· Tushirikiane na wenzetu, walio ndani ya Moyo huu ndio wote wanaomkiri Yesu kuwa Bwana, tena wanamcha/wanamwogopa Mungu.
· Tusali mara nyingi, tena tujifunze kusali vema. (Luka 22: 40). Tukisali tunawasiliana na Mungu ambapo anatupa ahadi zake nzuri; anatusikiliza, anatusaidia, anatushauri, anatuliwaza na kupokea masifu yetu - pia ni anatubariki. Tulete mipango, kazi, maamuzi na matokeo ya kazi zetu kwa Bwana naye atayabariki yote; na kutushauri jinsi ya kutumia neema zake kwa upendo zaidi kwa wenzetu.
· Tukitoka nje, turudi mara tugunduapo kosa hilo. Moyo wake upo wazi saa yoyote kutupokea.
· Tuwalee wapendwa wetu; watoto, marafiki n.k. kwa moyo huu. Tuwaache waonje utamu wake nao ....
Je? Unapenda kujua zaidi kuhusu Moyo Mtakatifu wa Yesu?
· Iwapo unapenda kujua zaidi kuhusu Moyo Mtakatifu wa Yesu, waweze kufanya haya:
· Soma Injili - Kuujua Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kuyajua Mapendo ya Mungu. Katika Injili yameonekana wazi zaidi. Hata hivyo sharti injili uielewe, uiamini na uipe nafasi ikufundishe au ibadili Moyo wako ufanane na wa Yesu.
· Soma Vitabu vingine mf. vya Watakatifu na vya Sala mbalimbali, Vitabu vyenye sala za Moyo Mtakatifu wa Yesu ni vingi.
· Shirikiana na wenzako katika kusali, kuwaza yahusuyo upendo wa Mungu, kupokezana vitabu na/au kanda za kaseti n.k.

Mtakatifu Margareta Maria wa Alakok
Kuna watu wengi sana walipanda baraka nyingi sana kutoka Moyo mtakatifu wa Yesu. Hata hivyo sasa navutwa kukueleza kuhusu Mtakatifu Margareta Maria wa Alakok. Mtakatifu Margareta Maria alipata maono ya Yesu, akijionyesha kwake kama Moyo Mtakatifu. Kwa sababu ya maono haya na ujumbe ulioambatana nayo, ndiyo maana sasa tuna michoro mingi ya Yesu akiwa amevaa joho lenye rangi nyeupe na nyekundu Moyo wake ukionekana kifuani.


Maono haya ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa Mtakatifu Margareta Maria yalitokea katika Kanisa dogo katika Konventi (Makazi ya Masista) ya Paray le Monio, huko Ufaransa, kati ya mwaka 1673 na 1675. Kristu alijionyesha kama Mtu-Mungu wa Moyo! Katika sikukuu ya Mtakatifu Yohana alipotokea alisema:
“Moyo wangu unampenda sana mwanadamu kiasi ambacho siwezi kuuzuia miali ya upendo huo; sharti niiache (miali) isafiri hata ng’ambo kwa njia yako (Mtak. Margareta Maria), na ijionyeshe yenyewe kwa watu ili kuwatajirisha kwa hazina ya neema wanayoihitaji ili kuokoka kutoka upotevu wa milele”.

Mwaka 1674, Kristu alitokea tena na kuonyesha mawazo yake kuhusiana na kukosa shukrani kwa watu wengi sana. Alisema: “Najisikia mateso kuliko nilivyoteseka siku waliyonisulibisha. Kama wangenirudishia (wakosefu) mapendo kidogo, nisingewaza yote ambayo nimewatendea, tena ningevutwa kuwatendea zaidi. Ila wananilipa mapendo yangu kwa ubaridi na machukizo”. Katika tokeo hili, Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliomba kuwe kunafanyika sala maalum Ijumaa na Alhamisi za kwanza za mwezi kwa malipizi ya dhambu na kwa kuwaombea wakosefu.

Funulio kubwa zaidi lilikuwa Juni 1675, ambapo alisema, “Tazama, Moyo huu uliowapenda wanadamu, hata umetoa yote na nguvu zote ili kumwonyesha mwanadamu mapendo yake. Tena, wanadamu walio wengi wananirudishia ukosemfu wa shukrani (ingratitude = kutokutosheka) kwa mambo yao yasiyo na umuhimu wala maana, kwa machukizo na makufuru yao na ubaridi wao wanaonionyesha katika sakramenti ya mapendo (ndiyo Meza ya Bwana). Lakini kinachoniumiza zaidi ni kwamba hayo yanatendwa na roho (watu) waliojiweka wakfu kwangu ... Naahidi kuwa Moyo wangu utawamwagia NGUVU ZA UPENDO wake wote wale watakaouheshimu au kuwashauri wengine wauheshimu”.

Katika matokeo hayo, Yesu aliahidi baraka nyingi kwa wale ambao watafunua mioyo yao kwa Moyo wake. Sista Margareta Maria alirekodi ahadi hizi katika barua zake, hasa ile “Ahadi Kuu” ya kufa katika upendo wa Kristu (urafiki na Kristu) iwapo atashika ibada ya Ijumaa tisa za kwanza za mwezi mfululizo. Kwa sasa ahadi hizo zimekusanywa pamoja, nazo ni hizi:
1. “Nitawapa neema zote wanazohitaji maishani mwao.
2. .Nitaleta amani katika familia/jamaa yao.
3. .Nitawatuliza katika taabu zao/huzuni zao.
4. .Nitakuwa kimbilio lao wakati wakiwa hai, hata baada ya kufa.
5. .Nitabariki kazi zao na shughuli zao zote.
6. .Wadhambi watapata bahari ya msamaha wa dhambi zao katika Moyo wangu/wadhambi watapata huruma katika Moyo wangu.
7. .Mioyo baridi itapashwa moto.
8. .Mioyo moto itavutwa kuelekea ukamilifu.
9. .Nitapabariki popote ambapo sura ya moyo wangu itawekwa na kuheshimiwa.
10. .Nitawapa Mapadre vipaji vya kugusa mioyo migumu.
11. .Wale watakaoeneza mvuto/upendo kwa moyo huu, majina yao yataandikwa katika moyo wangu.
12. Nawaahidi katika huruma kuu ya moyo wangu kuwa upendo wangu usiofifia utapewa kwa wote watakaoshiriki Komunio takatifu katika Ijumaa tisa za kwanza za mwezi, mfululizo - hawa hawatakufa bila kuungama dhambi zao kwanza - hawatakufa wakiwa wamechukizana nami; wala bila kupokea sakramenti muhimu. Moyo wangu wa Kimungu utakuwa kimbilio lao salama katika muda wao wa mwisho.

UPO WAPI KATIKA MOYO HUU?

NJE? NDANI? JUU? KANDO?

© Leander Kabutta

Saturday, June 13, 2009

KUSALI IBADA TAKATIFU YA MISA

Wengi tunasali Ibada Takatifu ya Misa.
Wewe pia nadhani unahudhuria Misa walau katika Dominika.
Lakini, umewahi kujiuliza maswali haya:
· Misa ni nini?
· Kwa nini tunahudhuria Misa?
· Misa ilianza lini?
Labda, ukiweza kuwaza maswali hayo na kuyajibu vizuri,
Msimamo wako kuhusu Misa utakuwa sahihi zaidi.
*************
Misa yote ni sala.
· Ni sala kubwa kuliko zote.
· Ni sala yenye utajiri kuliko zote.
· Ni sala iunganishayo watu wengi zaidi.
· Ni sala ya hisia zote - hudhuni, uchungu, furaha, Ibada, upendo, shukrani, maombi n.k.
· Ni sala ya Injili - ni Agizo la Yesu, ni sadaka ya Yesu, ni mazungumzo na Yesu, ni muungano na Yesu.
*************
Misa ni sadaka ya Yesu pale msalabani:
· Ni sadaka kubwa kuliko zote, kwani ni sadaka ya upendo kamili wa Mungu.
· Ni sadaka ambapo Mungu alimtoa mwanaye wapekee afe ili sisi tupone.
· Ni sadaka ambapo Mungu anamtoa mwanaye. Naye alikufa kwa ajili ya wote wa zamani, wa sasa na wa siku zote zijazo.
· Ni sadaka ya upendo wa Mungu.
· Je! Upendo wa Mungu una mwanzo? Mwisho Je?
· Hivyo ni Misa Takatifu ni sadaka ya milele...
· Tuunganikapo na Kristu katika sadaka hii, sisi tulio wa muda tunaungana na ya milele.

**************

Kiini cha Ukristu ni mapendo ya Kristu kwa wanadamu.
Kiini cha sadaka ya Misa ni Ekaristi Takatifu.
· Ekaristi Takatifu ni Kristu aliye Hai.

**************

Ekaristi Takatifu ni mapendo ya Kristu kwa wanadamu.
Yesu mwenyewe anajitoa sadaka kwa wanadamu, kwa namna ile ile aliyojitolea kuteswa na kufa pale msalabani.
Yeye mwenyewe anakuwa chakula na kinywaji cha roho kwa waumini wanaompokea.

****************
“Katika karamu ya mwisho Bwana Yesu ametunga sadaka ya Ekaristi kusudi sadaka ya msalaba iendelee siku zote mpaka atakaporudi. Aliliachia kanisa lake ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake kama chemchemi ya utakatifu, ishara ya umoja, na alama ya upendo; tena karamu ambayo Kristu ni chakula cha roho na mtu anajazwa na uzima wa Mungu akiahidiwa heri ya milele” (Mtaguso wa Pili wa Vatikani:47)
***************
Kumbe misa ni sadaka ya pekee!
Ni sadaka - ya upendo wa Mungu,
· iliyokamilisha sadaka zote za zamani, (“mimi sikuja kuitangua torati, bali kuikamilisha”).
· Ni sadaka ya pekee ambapo yeye mwenyewe (Kristu) ni kuhani (atoaye sadaka), altare (juu yake sadaka), altare (juu yake sadaka imewekwa) na mwanakondoo (atolewaye sadaka).

Tafakari sala hii:
Kweli ni vema na haki tukutukuze kila wakati, Ee Bwana, lakini hasa wakati huu, kwa shangwe kubwa zaidi, kwa kuwa Kristu ametolewa sadaka awe pasaka yetu. Yeye alipoutoa mwili wake msalabani. Naya anapojitoa kwa ajili ya wokovu wetu, yeye mwenyewe alijifanya kuwa kuhani, altare na mwanakondoo. Na kwa sababu hiyo, Watu wote wanaitukuza sikukuuu ya Pasaka kwa furaha kubwa popote duniani. Nao Malaika wote wa Mbinguni wanaimba wimbo wa kukutukuza, wakisema bila mwisho:”
(Utangulizi - sala ya Ekaristi- Pasaka V)


Maisha ya Yesu na sadaka ya Misa
Yohana 4: 13 - 14
“Yesu akamjibu (mwanamke Masamaria), kila anayekunywa maji haya (ya kisima cha Yakobo ) ataona kiu tena. Lakini atakeyekunywa maji nitakayompa, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa chemichemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa Milele’’
Yohana 6 : 35
“Yesu akawaambia (Wayahudi waliojaa sinagogi la Kafarnaum) Mimi ndimi mkate wa uzima. Anakuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe ”.
Yohana 6: 41
“. . basi Wayahudi wakaanza kunung’unika kwa kuwa alisema: Mimi ni mkate ulioshuka kutoka Mbinguni”.
Yohana 6: 50 - 51
“Huu ndio mkate ushukao kutoka Mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa. . Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka Mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninautoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu”
Yohana 6: 53
“Yesu akawaambia, kweli nawaambieni, msipokula mwili wa mwana wa mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uzima ndani yenu”.
Yohana 6: 54
“Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu, anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho”.
Yohana 6: 55
“Maana mwili wangu ni chakula cha kweli na damu yangu ni kinywaji cha kweli”.
Yohana 6: 56
“Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, anakaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake”.
Yohana 6: 57
“Baba aliye hai alinituma, nami naishi sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu”.
Yohana 6: 58
“Basi huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliokula baba zenu, wakafa. Aulaye mkate huu atakuwa na uzima wa milele”.


Zoezi:
Tafakari asehemu hizo za Injili ya Yohana, kipengele baada ya kipengele.
Baada ya kutafakari, soma Yohane 6: 35 - 58 kwa sauti. Unaiona picha halisi ya sadaka ya Ekaristi
Sali - mshukuru Yesu wa Ekaristi, kwa kutupa zawadi hii - ili tuwe naye daima.

Wewe na Ibada ya misa
Ibada ya Misa ni kama mti mzuri utoao maua na matunda mazuri. Majani na maua yake hupendeza. Watu huchuma maua yake wakapamba nyumba zao. Wengine huchuma matunda yake wakala wakashiba, tena katika matunda hupata mbengu wakazipanda zikaota miti mingine. Wakati wa jua kali, watu wengine hupata kivuli chini ya mti huo; na mvua inyeshapo, wengine hupata kinga chini ya mti huu. Nyuki nao huvutiwa na maua ya mti huu - katika maua yake wanapata vifaa vya kutengeneza asali na nta.
Fikiri: Wewe ni nani katika mti huu?
· Mtu achukuaye maua yake na kupanba nyumba yake?
· Mtu achumaye matunda na kuyala; kisha mbegu zake akazitupa bila kujali zitakapoanguka?
· Mtu achumaye matunda na kuyala; kisha mbegu zake akazipanda penye ardhi nzuri nazo zikaota kuwa miti mingine?
· Mtu apataye kivuli chini ya mti huu?
· Mtu apataye apataye kinga ya mvua chini ya mti huu?
· Nyuki apataye kutoka maua ya mti vifaa vya kutengeneza asali na nta?
· Au mtu afaidikaye na asali na nta ya nyuki?

Fikiri: Mti huu ni mali hasa ya nani?
* Nani awezaye kusema mti huu ni mali yake kati ya hao saba?

Hatima
: Pata wazo kuwa Ibada ya Misa ni upendo wa Mungu.
Upendo wa Mungu ni kwa watu wote. Hivyo Sadaka ya Misa ni ya watu wote; ni moja, na atolewaye ni mmoja, ndiye Yesu Kristu. Hutupa faida za muda (kama mti ulivyokuwa katika mapato, kivuli na kinga ya mvua), pia hutupa faida zidumuzo (kama ulivyo mti katika maua na matunda). Tunda la mti huu ni Ekaristi Takatifu.

Sadaka ya Misa: Maua

Hakika Ibada ya Misa ni Ibada ya kupendeza macho na mioyo, hasa ikijumuisha tamaduni zetu (inculturation).
Fikiri vitu hivi:
· Watu wenye nia njema - matajiri waliovaa nguo nzuri na maskini zile nzuri zaidi walizonazo.
· Mapambo ya Altare na kanisa: vitambaa, maua, mishumaa n. k.
· Nyimbo nzuri zenye kupendeza ziambatanazo na vigelegele, vinanda, tarumbeta, kengele n. k.
· Maandamano ya Padre na watumishi, maandamano ya matoleo n. k.
· Sala za Liturgia zenye kugusa moyo na kuamsha moyo wa Ibada.

Vyote hivi hupendendeza; hupendeza kama ua, huvutia kama ua na wote washirikio huondoka na mioyo iliyopendezeshwa. .
Jichunguze/chunguza:
Ni kipi kinachokuvutia zaidi katika Ibada ya Misa? Ni kipi kinachowavutia watu, kwa mfano kufunga ndoa zao katika Ibada ya Misa japokuwa wao hawana mazoea ya kwenda kanisani?
***************

Sadaka ya Misa: Matunda
· Sayansi yatuambia kuwa maua hugeuka kuwa matunda hatimaye. Kile kilichowavutia watu kwa sura na harufu yake, baadaye huwa shibe yao.
· Wajao katika Ibada ya Misa hushibishwa ubinadamu wao. Ni kusanyiko la watu ambapo weupe kwa weusi, wake kwa waume, matajiri kwa maskini huwa sawa wakisoma neno moja, wakisikilizana sauti ya mmoja, wakikiri imani moja, wakipata baraka ya mmoja na kula chakula kimoja ambacho huwafanya mwili mmoja katika Mungu mmoja. Ni sadaka ya UMOJA.
· Wao katika Ibada ya Misa hushibishwa roho zao kwa neno wa Mungu (Liturgia ya Neno) na sakramenti ya Ekaristi (liturgia ya Ekaristi). Kristu aliye hai hujionyesha katika maisha yao kwa njia ya mahubiri tena huonyesha upendo wake na utashi wake wa kuwa nasi daima kwa njia ya komunio Takatifu, na huonyesha dhamiri yake ya kusamehe na kututakasa (na hakika hututakasa) kwa njia ya damu yake takatifu.
· Umungu wake huonekana: Fikiri alivyo wa ajabu huyu Yesu wa Ekaristi: Mkate mmoja - watu wengi, nchi mbalimbali, zamani, sasa na baadaye. . . Lakili Kristu ni yule yule mmoja hagawanyiki, hapungui wala hazeeki wala kuoza. . . huwepo kwa yeyote apendaye kumpokea wakati wowote, popote. . .

***************
Sadaka ya Misa: Mbegu
Mara nyingi mbegu huwapo katika tunda. Katika sadaka ya Misa pia kuna mbegu, mbegu za NENO LA MUNGU. Mpandaji mkuu ni KRISTU mwenyewe. . . . lakini anatualika wote tufaidikao na matunda pia tuwe wapandaji wasaidizi.
· KRISTU hupanda neno lake katika mioyo yetu, neno hili hukua, likaota mizizi. . . maua yakatokea na kutupendezesha mbele za Mungu na wanadamu na kuwavutia watu kwetu ambao sisi huwaelekeza kwa KRISTU.
· Matunda hutokea nasi hufaidi zaidi. Mbegu tuzipatazo kutoka katika matunda huzipanda kwa wengine . . . Je! baada ya kupanda inatupasa kusaidia palizi, kunyweshea n. k. hadi maua na matunda yapatikane? Jadili nafsini mwako.
· Watoto wetu huwaleta katika Ibada ya Misa ambapo nao kama mashamba:
1. Hutayarishwa kwa kilimo na kutiwa mbolea - mafunzo na kitubio.
2. Hupandwa - neno na sakramenti mbalimbali na
3. Hutunzwa kwa sakramenti na visakramenti mbalimbali hadi matunda yanapatikana.

· Sote sisi hushirikishwa na Kristu katika kutayarisha shamba, kupanda, kutunza mimea. . . nasi hufaidika na matunda sasa. . . na milele. . .
Sadaka ya Misa yatushirikisha sote upanzi wa Kristu:
· Sisi hupanda pamoja na Kristu.
· Sisi hutumwa kupanda pamoja na Kristu.
· Sisi pia tu udongo . . . ndani yetu mbegu hupandwa.

Kwa nini tunazungumzia sisi wala si mimi?
Jibu: Sadaka ya Misa ni ya wengi si ya mmoja. Yawahusu walio Mbinguni na walio Duniani; walio taabani vitandani na walio kuzimu; walioishi, wanaoishi na watakaoishi; waamini na wasioamini; waasi na waalimu wa kanisa; watu wote. . . ambao Kristu aliwafia msalabani. Ni sadaka KATOLIKI.
***************
Sadaka ya misa: Faraja
Yule aliyejikinga kwa jua na mvua chini ya mti alipata faraja. Ibada ya misa ni uwepo wa Mungu katika ukamili wa upendo wake, huruma yake na utukufu wake.
Kuuhisi uwepo wa Mungu hakika huleta faraja kubwa ya moyo:
· Dhambi zetu hufutika mbele ya upendo na huruma ya Mungu.
· Elimu, sayansi na Teknolojia hushushwa na kuonekana kama mawazo mazuri ya mtoto mtundu na mbunifu mbele ya babaye ajuaye yote.
· Uzito na taabu za duniani huonekana vitu vidogo sana mbele ya msalaba wa Kristu.
· Kifo kwa wakiogopao hushindwa kabisa mbele ya Kristu mfufuka aliyeyashinda mauti. Si tishio tena kwao!
· Kifo kwa wamtumainiao huwa furaha ya kueandelea kuwa naye. Misa yatudhihirishia waamini kuwa tu wake tuwapo hai pia tufapo. Tunakuwa kama fedha iliyohamishwa kutoka mfuko mmoja wa vazi kwenda mwingine. . . na bado tunabaki mali ya mwenye vazi, tena ndani yake.
· Utajiri huwa kipaji cha kusaidia maskini; na umaskini huwa shule ya kujifunza kumtegemea na kutambua upendo na huruma zake.
Ibada ya misa ni faraja kwa wote. Yeye mwenye Ibada hii alisema:
“Njooni kwangu ninyi nyote mnaosumbuka na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11: 28).
“Nendeni mkawambie. . . . . mambo mnayoyasikia na kuyaona:
Vipofu wanona,
Viwete wanatembea,
Wenye Ukoma wanatakaswa na
Viziwi wanasikia tena;
Wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema,
Heri mtu yule asiyekuwa na mashaka nami”. (Mathayo 11: 4 - 6)
Fikiri furaha na faraja waipatao:
· Vipofu wanapopata tena kuona. Jiweke katika nafasi ya kipofu fulani. . . .
· Viwete wanaopata kutembea . . . jiweke katika nafasi ya kiwete mmoja wa hao - kiasi gani utarukaruka kwa furaha!?
· Mwenye ukoma anayetakaswa . . .
· Kiziwi anayepata tena kusikia . . .
· Mfu anayepata uzima tena . . .
· Maskini anayeahidiwa UTAJIRI WA MILELE ,,,

ZOEZI DOGO: TAFAKARI MATHAYO 11: 4 - 6

2 comments:

  1. Asante father kwa post nzuri hivi.... Naendelea kuisoma polepole ila so far nimefarijika nayo sana jinsi inavyoelimisha. Mimi niko ndani ya Moyo Mtk.wa Yesu (mwanashirika mlei). Nitaendelea kusoma blogu yako yote. Mungu akutie nguvu baba yangu.

    ReplyDelete
  2. Asante sana father, umeeleza vizuri sana na nimejifunza mengi.. ๐Ÿ™ na Moyo wa Yesu utazidi kukukirimia neema na hazina zake.. Usifiwe Moyo wa Yesu unaotupenda na kutupa Amani.. Mimi niko ndani ya shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu(Mlei) asante Baba

    ReplyDelete